Wednesday, September 8, 2010

Azam inaonesha njia

LAITI vilabu vyote Tanzania vingelikuwa vinamilikiwa na mtu mmoja au watu walionunua hisa na hivyo kuwekeza kwenye timu husika mchezo wa mpira leo Tanzania ungelikuwa ni eneo zuri la ajira na uzalishaji kipato kwa wawekezaji, wachezaji na watoza kodi.

Michezo hapa Tanzania ina bahati mbaya ya kuchukuliwa kama vile ni sehemu ya siasa, vyama vya siasa na serikali. Kutokana na hili viongozi wabovu walikuwa wakivumiliwa ili mradi wana utiifu kwa chama fulani cha siasa.

Katika miaka ya sasa lazima michezo yote ikiwemo mpira wa miguu iwe na mwelekeo wa kiuchumi, kibiashara na kiajira kwa maana ni wale watakaokuwa wanacheza mpira au wanaowekeza katika mpira ndio wanaotakiwa kufaidika ikiwemo kutajirika kutokana na mchezo wanaoucheza.

Lazima ieleweke kujifunza michezo ni sawasawa na kujifunza elimu nyingine yoyote na sio mchezo. Baada ya mtu kujifunza michezo lazima ajiajiri au aajiriwe kwa kipato kinacholingana na kujitolea kwake kujiendeleza katika eneo husika.

Ilivyo hivi sasa kwa sababu thamani ya wachezaji wetu wanapotoka vijijini huonekana ni ndogo kwa sababu siasa zetu za nchi za Kiafrika ni za 'kiapartheid' kati ya maeneo ya mashambani/vijijini na yale ya mijini basi tunawanyonya toka huko hadi wakifika mjini na kuwadharau kama vile hatutambui wala kuelewa kuwa kama sio wao hapawezi kuwa na Yanga, Simba, Manyema. Pan Africa, Toto Africa, Malindi na kadhalika.

Azam kwa hakika imeonesha njia kwa kuona kuwa mchezaji kama Ngassa angalau kwa viwango vyetu vya Kitanzania ana thamani ya dola hamsini elfu. Pongezi sana wamiliki wa Azam.

Tunadhani huu ni mwanzo tu na kama Abramov alivyofanya na Chelsea tunaamini kuwa Azam itakusanya wachezaji wazuri sio tu toka Tanzania bali pia toka Congo Kinshasa, Zambia, Malawi, Msumbiji, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ili kupata timu ya wachezaji itakayomaliza aibu ya timu za Tanzania kuwa zinashindwa kirahisi na zile za nchi za Afrika Magharibi na kaskazini. Hili linawezekana, lakini linahitaji kuwekeza na kuwawezesha wanaokabidhiwa kazi hii kubwa ya kufuta machozi ya mashabiki wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Matatizo ya vilabu visivyokuwa na mmiliki mmoja au wanahisa ni kwamba wale wenye uroho wa madaraka wana kawaida ya kugombea vyeo na baada ya hapo kazi yao inakuwa sio kuwekeza na kuendeleza soka, bali ni kula na kudidimiza klabu na kujipangia mambo mradi yaende kiswahili swahili kwa kudra ya Muumba bila kutambua kuwa michezo katika dunia ya leo ni jambo la sayansi na teknolojia.

Viongozi wa namna hii si aibu na hasara kwa klabu tu bali ni maafa kwa taifa. Ninaamini wakati umefika wa klabu kumilikiwa na mtu binafsi au kundi la wenye hisa ambao hawatasita kumtimua meneja au kocha pindi waonapo kashindwa kufanya kile walichokubaliana.

AZAM kwa wengi wasiojua inaashiria mwanzo wa kifo cha Simba na Yanga kama timu zinazoyumbishwa na matajiri wasiozimiliki, viongozi walasana, wachezaji mamluki na vikongwe wasio na mwamko wa ushindi wala umaarufu wa kimichezo bali kujaza matumbo na mifuko yao kwa hicho kidogo wanahodanganywa nacho.

Umiliki wa timu au klabu na wenye hisa au tajiri mmoja utalazimisha kuwa na menejimenti ya kweli kweli kisoka/kimichezo, kutakuwa na mipango na bajeti na haitakuwa rahisi kwa mwanasiasa yeyote, ngazi yeyote kuingilia klabu katika maamuzi na mipango yake. Wengine igeni haraka kabla hamjafa na kusahaulika kama waliowatangulia.